Monday, September 3, 2012

Sitta ageukwa CCM, Aibuka kumjibu Dk. Slaa,


SIKU moja baada ya Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa kumrushia kombora zito Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Hamis Mgeja amemtaka waziri huyo na wabunge wengine 55 wapime, watafakari na hatimaye wachukue hatua kwa kuondoka ndani ya CCM.
Mgeja ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, amesema tuhuma zilizotolewa na Dk. Slaa dhidi ya Sitta na wabunge hao, zinathibitisha jinsi kiongozi huyo na wenzake walivyo wasaliti ndani ya chama chao na serikali, na kwamba kitendo cha kuigeuza ofisi ya spika kuwa kijiwe cha kupanga uhaini na usaliti ndani ya CCM hakivumiliki hata kidogo.
Mgeja alitoa kauli hiyo jana jijini Mwanza, alipozungumza na waandishi wa habari kwa lengo la kumpongeza Dk. Slaa kwa kufichua uozo wa Waziri Sitta na wenzake hao. Alisema Dk. Slaa ameisaidia CCM kutambua viongozi wake wanaokisaliti.
"Nianze kwa kumpongeza Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Slaa kwa kufichua madhambi ya Samuel Sitta. Huyu mtu (Sitta), ni hatari sana katika maendeleo ya chama chetu.
"Dk. Slaa ametueleza jinsi Sitta alivyotumia ofisi ya spika kama kijiwe cha kutaka kukisaliti chama chetu na kuanzisha CCJ. Huyu mtu ni hatari sana... tunaomba CCM imtose yeye na wabunge hao 55 maana uroho wao wa madaraka unaweza kuigharimu CCM.
"Kwa kashfa hii nzito dhidi yao, namshauri wapime, watafakari na hatimaye wachukuwe hatua. Pia nawashauri kwanza watubu na kuomba radhi chama na wana CCM wote, au wajiengue kwa hiari yao bila shuruti, ili walinde heshima yao. Wasingoje kuhukumiwa na wanachama," alisema.
Mjumbe huyo wa NEC na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga aliyejipambanua kupiga vita ufisadi na vitendo viovu ndani na nje ya CCM, alisema historia ya Waziri Sitta inajionesha wazi kwamba ni 'mkorofi na msaliti mkubwa', kwani mwaka 1966 akiwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alishiriki maandamano hadi Ikulu kupinga sheria ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Alisema katika harakati zao hizo za kupinga sheria hiyo iliyotaka kila mwanafunzi wa Chuo Kikuu lazima ajiunge na Jeshi la Kujenga Taifa, Baba wa Taifa wakati huo akiwa Rais wa nchi na mkuu wa chuo hicho, alilazimika kumchapa viboko Sitta kutokana na usaliti wake huo kwa serikali.
Mgeja alisema mbali na kufanya maandamano hayo, Sitta na wenzake ambao wengine ni marehemu kwa sasa walikuwa na mabango yenye ujumbe mkali kwa serikali, ukiwemo uliosema 'Onyo kali na la mwisho kwa serikali', na kwamba alikuwa akiipinga pia Serikali ya Baba wa Taifa huku akiusifu uongozi wa kikoloni.
"Huyu Sitta ambaye leo hii anawadanganya watu, kipindi hicho akisoma Chuo Kikuu alikuwa akiipinga serikali na kudai afadhali serikali ya kikoloni. Tusipoamini leo usaliti wake huu tunasubiri hadi aje shetani atuambie usaliti wa Sitta ndipo tuamini?
"Za mwizi ni 40, ndiyo maana tumeambiwa toka mwaka 2005 hadi 2010 huyu Sitta amekuwa akikisaliti chama chetu kupitia Bunge alilokuwa akiliongoza. Tunataka chama kimtose na kisiwaonee haya wasaliti hawa wakubwa. Wasipoondoka kwa hiari yao wataondolewa kwa nguvu ya wanachama wa CCM,” alisema.
Alimtuhumu pia Waziri Sitta kwa kauli zake za kulalamikia serikali bila kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayolikumba taifa, na alimtaka ataje jinsi alivyoisaidia serikali kupunguza tatizo la ajira kwa vijana, mfumuko wa bei, ufisadi na mambo mengine ndani ya chama na serikali.
Kwa mujibu wa Mgeja anayedaiwa kuanza kuundiwa mbinu chafu za kutaka kuangushwa katika kinyang'anyiro cha uenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga na kundi la kigogo mmoja anayetajwa kutaka kugombea urais mwaka 2010, tuhuma hizo dhidi ya Waziri Sitta zimekisaidia maradufu chama, kwani siyo Dk. Slaa pekee aliyewahi kumshutumu kiongozi huyo kwa usaliti ndani ya chama.
Alisema yupo tayari kusulubiwa, kutolewa kafara au kufukuzwa na chama kwa kusema ukweli daima, kwani anayasema hayo kwa kufuata kiapo cha katiba ya CCM.
Sitta amjibu Dk. Slaa
Waziri Sitta amemjibu Dk. Slaa akimwita dikteta na asiye na uvumilivu na kwamba ana hulka ya kujisikia kuwa mawazo yake hayapingwi.
Waziri Sitta amemwita Dk. Slaa kuwa ni mzushi, asiyeogopa kusema na kupindisha mantiki ya jambo ili tu kushinda hoja.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyoitoa jana, Sitta alisema amesikitishwa na kauli hizo za Dk. Slaa alizoziita za jazba na mwangwi wa kiwewe alipokuwa Iringa juzi hadi akafikia hatua ya kumwita mnafiki, mwongo, mtu wa hatari n.k
“Hali hii inatia shaka juu ya uwezo wa kiongozi huyo wa kisiasa kuhimili kukosolewa ambayo ni sifa muhimu ya maisha ya mwanasiasa yeyote hususani anapojinadi kuwa anaweza kuchukua madaraka ya kuiongoza nchi.
“Iweje mtu aliyenibembeleza nigombee urais kupitia chama chake mwaka juzi leo aseme sifai kuongoza hata kata kwa sababu tu nimetamka ukweli juu ya udhaifu wa chama chake cha siasa?” alihoji Sitta.
Alieleza kuwa aliyoyasema Karagwe majuzi katika uchambuzi wake wa vyama vya siasa nchini ni kwamba CHADEMA wamekuwa hodari wa kukosoa na kuishambulia CCM na serikali zake lakini wanasahau kuwa ili wawe mbadala kwa kuiongoza nchi hawana budi kurutubisha safu yao ya uongozi na uwe na watu wa kutosha kuweza kushika madaraka ya ngazi mbalimbali.
“Kuukataa ukweli kwamba safu ya uongozi wa CHADEMA ni nyembamba ni kujidanganya tu. Kupita mikoani kutangaza kwamba matatizo yote ya wananchi yanatokana na CCM ni kazi rahisi na ina mvuto wake kisiasa, lakini mwanasiasa makini hana budi kwenda mbele zaidi ya hapo,” alisema Sitta katika taarifa yake.
Alimtaka Dk. Slaa kueleza wapiga kura mipango ya chama chake inayoeleweka na inayotekelezeka na iliyo makini kukabiliana na changamoto mbalimbali za maendeleo ya nchi.
Amgwaya Mbowe
Kuhusu Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, Sitta alionyesha kumgwaya akieleza kuwa katika hotuba yake hakukejeli uzoefu wa kiongozi huyo wala hakusema ni mcheza disko.
“Niliuchambua wasifu wa viongozi wa CHADEMA na kutamka uzoefu wa Mhe Mbowe katika vitega uchumi vya burudani, hii siyo kudharau bali ni kutamka ukweli tu.
“Huwezi kuuelezea wasifu wa Mhe Mbowe bila kuelezea mchango wake mkubwa katika tasnia ya burudani,” alisema.
Alieleza kuwa mmoja wa marais maarufu wa Marekani, Ronald Reagan, alikuwa ni mcheza sinema. Na hapa Tanzania kulikuwa na Rashidi Kawawa (sasa marehemu) ambaye alianzia katika tasnia ya uigizaji hivyo Mbowe au Dk. Slaa wanaweza wakawa marais wa nchi kwa maana ya kupigiwa kura za uchaguzi wa demokrasia.
“Kumudu au kutoyamudu madaraka hayo ni suala tofauti. Tathmini yangu ilihusu safu nzima ya uongozi wa CHADEMA kwa ujumla wao. Ni safu nyembamba mno,” alisema Sitta.
Kujiunga na CHADEMA
Kuhusu suala hilo, alisema CHADEMA walifanya jitihada ya kumshawishi aingie kwenye chama hicho kwenye uchaguzi wa mwaka 2010 na ili awe mgombea wao wa urais.
“Jambo hili nililitafakari na kutafuta ushauri kwa watu wangu wa karibu na nikabaini kwamba; CHADEMA wana migawanyiko yao ya uongozi tena ni ya hatari kwa sababu ni ya kikanda za nchi – yaani nani anatoka wapi.
“Kutokana na yaliyomo katika ilani yao ya uchaguzi 2010 – 2015 nilibaini mambo ya kiitikadi ambayo siyakubali kama vile sera ya majimbo,” alisema Waziri Sitta.
Alisema sera ya majimbo inawezekana katika nchi ambazo ni tajiri na pia isiyo na tofauti kubwa ya hali ya maisha baina ya kanda mbalimbali za nchi kama vile Marekani.
Sitta alisema kuleta majimbo Tanzania ambako kuna tofauti kubwa za kimaendeleo baina ya Kaskazini, Mashariki, Kati, Kusini na Magharibi ni kusababisha nchi ichanike vipande vipande.
Kuhusu CCJ
Alisema kama ilivyo kawaida kwa vyama vya siasa kutafuta wagombea bora, CCJ ni miongoni mwa vyama vilivyomtafuta na baadhi ya wanasiasa wengine wakati wa maandilizi ya uchaguzi mkuu.
“Jambo hili si la siri wala la ajabu na nimelizungumza hili mara nyingi. Isitokee katika mfumo wa vyama vingi vya siasa mtu kutoka chama kumoja cha siasa na kujiunga na chama kingine haiwezi kusemwa kuwa ni uhaini,” alisema Sitta.
Alisema kama angeridhika na mambo yao angejiunga na CCJ mwaka 2010 lakini hakufanya hivyo.
Alieleza kuwa ni uzushi usio na msingi kumuhusisha na uanzishaji wa chama hicho kwani waanzilishi wa chama hicho cha siasa wanajulikana na wapo hai lakini alieleza kuwa ni haki ya kikatiba ya kila Mtanzania kuanzisha au kujiunga Binafsi na chama chochote cha siasa. Hata hivyo mmoja wa waanzilishi wa CCJ, Fred Mpendazoe, alimtaja Sitta kama mwasisi mwenzake ambaye hakutaka kujitokeza hadharani kabla chama hakijapewa usajili wa kudumu.
Kuhusu madai yake ya kutamka kwamba angehamia CHADEMA na wabunge wa CCM 55 alisema hizo ni porojo za Dk. Slaa kama ulivyo usemi ‘ningeihama CCM siku chache kabla ya kuvunjwa Bunge la 9’.
“Inashangaza kwa Dk. Slaa kukejeli uendeshaji wa Bunge la 9 ambalo ndilo lililowapa fursa watu kama yeye kujulikana na kujipatia umaarufu,” alisema Sitta.

No comments: