Ndugu wananchi hivi majuzi Chama Cha Mapinduzi Mkoa
kilitoa maelekezo ya kuwa serikali itoe ufafanuzi juu ya miradi ya uwekezaji
inayotekelezwa katika eneo lake. Aidha
Mkuu wa Mkoa ameniagiza kutoa taarifa
hiyo kupitia tamko hili.
Napenda kutoa taarifa ya ufafanuzu kama ifuatavyo:
1. UTANGULIZI:
Wazo la kuanzisha miradi ya uwekezaji katika
Manispaa ya Bukoba, lilitokana na azima ya kuongeza mapato ya Halmashauri
kufikia bilioni Nne (4 bilioni) ifikapo
mwaka 2015. Aidha nguvu hii ya
kiuchumi ingewezesha Halmashauri ya Manispaa kufikia ndoto yake ya kupata hadhi
ya kuwa Jiji ifikapo au kabla ya mwaka 2020.
Katika kufikia malengo hayo viupaumbele vya Halmashauri,
mpango mkakati wa uendelezaji wa mji wa Bukoba wa mwaka 2008 – 2028
ahadi za Mhe. Mbunge katika
Uchaguzi Mkuu mwaka 2010, ahadi za Rais
na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2010 – vilizingatiwa.
Miradi iliyoainishwa kutekelezwa ni kama ifuatavyo:-
1.
Ujenzi wa Kiteuga
Uchumi
2.
Upimaji wa viwanja
5000
3.
Ujenzi wa Stendi
ya mabasi Nyanga.
4.
Mradi wa Kuosha Magari.
5.
Ujenzi wa Soko
Kuu.
6.
Uendelezaji makazi
Kashai na Miembeni.
7.
Ujenzi wa Chuo cha
Ualimu
8.
Ujenzi wa Kituo
cha Maarifa (Center of excellency)
9.
Ujenzi wa bwawa la
maji kwa ajili ya Utalii
Miradi minne ya mwisho bado ipo katika hatua ya
kufikiriwa na hivyo taarifa yangu itajikita katika miradi 5 iliyoanza
utekelezaji.
Ili kufanikisha utekelezaji wa miradi hii tulizingatia ushirikishwaji wa
sekta binafsi – (PPP) kama ilivyo
matakwa ya Kisera. Aidha, kwa madhumuni ya kuongeza ufanisi katika kufikia
malengo tumeingia mikataba ya makubaliano
na Shirika la Mzinga na Kampuni ya Procurement and Technical Service Limited
(PTSL).
Maeneo
ya Ushirikiano
1. Shirika la Mzinga -
(Mzinga Co operation)
Hili ni Shirika la Jeshi la Wananchi wa Tanzania
lililopewa dhamana ya kushirikiana na
taasisi za Serikali katika masuala ya
mchakato wa maendeleo kwa kutoa huduma za kiushauri na kiufundi. Makao makuu yake yako Morogoro.
2. Kampuni ya PTSL - (Procurements and
Technical Services Ltd)
Hii ni Kampuni iliyoandikishwa chini ya Sheria ya ma
kampuni kufanya shughuli za biashara ikiwa ni pamoja na kutoa ushauri wa
kuanzisha na kutafuta mitaji ya shughuli za kibiashara aidha, Kampuni hii
imeshiriki katika kuandaa makongamano mbalimbali kama maonesho ya ALAT Taifa na
ALAT Mkoa Kagera. Makao makuu ya Kampuni
hii yako Dar es Salaam.
Mchakato wa kuwapata washirika wa maendeleo ulipata
baraka za Baraza la Madiwani katika kikao chake cha tarehe 10/5/2011.
A: KITEGA UCHUMI
Halmashauri imepanga kujenga jengo la Kitega Uchumi
lenye ghorofa 10 katika eneo la stendi ya sasa . Mradi huu unatarajiwa kutekelezwa baada ya
stendi kuhamia Kyakailabwa.
i)
Utekelezaji hadi sasa:
·
Kutafuta Mtaalam
Mshauri kwa ajili ya kuandaa andiko
la awali la maradi. Halmashauri
ilimteua kwa njia ya zabuni “ARCH PLAN INTERNATIONAL” ya Dar es Salaam kufanya
kazi hiyo kwa thamani ya TShs. 109 milioni na tayari amelipwa TShs. milioni 10.
·
Mkandarasi
ameshaandaa andiko la awali na kukamirisha
tathimini ya awali inaonesha jengo hilo litagharimu Shilingi bilioni 11.
·
Halmashauri kwa
kushirikiana na Mkandarasi Mshauri imewasiliana na NSSF kuhusu uwezekano wa
kufadhili mradi huu.
-
NSSF walitaka
Halmashauri kupata dhamana ya Serikali, ambapo Serikali ilikubali kuipa
Halmashauri Udhamini kwa njia ya “Letter of Comfort” badala ya “Guarantee”.
-
Halmashauri
imeshawasilisha uamuzi wa Serikali kwa NSSF na mazungumzo yanaendelea.
Changamoto:
1.
Mwelekeo na
mazungumzo na NSSF umepungua kasi, hii inatokana na NSSF kutopendelea utaratibu wa Letter of
Comfort badala ya Guarantee.
2.
Kuchelewa kuhama
kwa standi kutoka eneo la sasa kwenda Kyakailabwa.
Ufumbuzi
wa Changamoto:
1.
Kuendeleza mazungumzo
na NSSF ili waweze kufadhili mradi huo.
2.
Kuendelea kuuza
mradi huo kwa wafadhili wengine ili kupata fedha za kutekeleza mradi.
3.
Kuongeza kasi ya
kuhamisha standi.
B: MRADI WA VIWANJA 5000
Mradi huu
ulizaliwa na wazo kutoka kwenye Mpango Mkakati wa uendelezaji wa mji wa Bukoba wa mwaka 2008
– 2028.
Mpango huo, ulipendekeza upimaji viwanja vya
kutosheleza watu 40,000. Sawa na
viwanja 8,000. Kwa wastani wa watu 5 kwa
Kaya. Katika Kata za Nyanga, Buhembe,
Nshambya Kahororo, Kashai, Kitendaguro na Ijuganyondo.
i) Maandalizi
ya awali ya mradi
·
Halmashauri
iliandaa andiko la mradi na kuwasilisha katika Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya
Makazi ili kupata fedha za kulipa fidia na kupima. Andiko lilionesha uhitaji wa Shilingi za
Kitanzania bilioni 1.6 (TShs. 1.6 bilioni).
·
Kutokana na
Halmashauri nyingi kushindwa kurejesha fedha kwenye mfuko wa wizara wa upimaji
viwanja, wizara ilishindwa kupata fedha kwa wakati huo kutupatia kwa ajili ya
kutekeleza mradi huu.
·
Halmashauri
ilianza juhudi za kutafuta fedha kutoka vyombo vingine vya fedha ili kutekeleza
mradi huo.
·
Katika harakati
hizo Halmashauri ilifanikiwa kuingia mkataba wa makubaliano na Mfuko wa Dhamana
Tanzanaia (UTT) ili kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi huo. Mkataba huu upo kwa mfumo wa ushirikiano
(joint venture).
Halmashauri iliingia mkataba wa makubaliano na UTT
kutekeleza mradi huo mnamo tarehe 20/6/2011.
Aidha, wataalamu wa Halmashauri
na wataalamu wa UTT walipitia upya Andiko la Mradi ili kupata uhalisia wa
gharama za utekelezaji wa mradi. Gharama
za mradi zilifikia Shilingi za Kitanzania bilioni 2.6 (TShs. 2.6 milioni).
(ii) Utekelezaji wa Mradi
Utekelezaji mradi ulianza baada
ya mkataba kusainiwa, kazi
zifuatazo zimefanyika:-
1.
Kufanya tathmini
na kulipa fidia kwa wananchi 1,000 wenye thamani ya Shilingi bilioni 2.2 (TShs. 2.2 bilioni).
2.
Kupima viwanja
4,898 kwa gharama ya TShs. 290,000,000/=.
Kazi hii imefanywa na Chuo cha Ardhi Morogoro.
3.
Kufungua barabara
zenye urefu wa Km. 54.01 kwa gharama ya
TShs. 366,371,818.00. Kazi hii imefanywa
na mkandarasi Kajuna Investment.
4.
Kuuza viwanja
ambapo mradi unategemea kupata Shilingi bilioni 8 (TShs. 8 bilioni) ambapo hadi
tarehe 27/11/2012 kiasi cha TShs. 3,064,532,000.00 kimekusanywa kutokana na
uuzaji wa viwanja na kuwezesha kurejesha UTT Shilingi bilioni 2.54 (TShs. 2.54
bilioni) ambazo ni mtaji mama wa utekelezaji wa mradi. Fedha zote za mradi zimepokelewa na
kuhifadhiwa kwenye akaunti ya pamoja ya mradi
(BMC and UTT) iliyofunguliwa Benki ya Posta.
-
Viwanja vitaendelea
kuuzwa hadi Februari, 2013 ambapo tunategemea kufunga mradi na kugawana faida kwa uwiano wa 60% (UTT) na 40% (BMC).
·
WAKATI
WA KUUZA VIWANJA
Katika uuzaji viwanja kuna
makundi mawili maalumu yaliyowekewa utaratibu mahususi wa kununua viwanja:
1. Wale wenye maeneo
yaliyotwaliwa.
- Hawa watapata punguzo la Shs. 400,000/= kwa kiwanja kimoja miongoni mwa viwanja atakavyonunua
vyenye ujazo mkubwa (High Density)..
2. Wale waliochangia
gharama za upimaji zamani.
- Hawa watapata punguzo la thamani ya fedha ya sasa itakayo kokotolewa kutokana
na mwaka waliochangia na kiasi walichochangia.
Aidha wale ambao hawatakuwa tayari kununua viwanja katika kundi hili
watarudishiwa fedha zao kwa thamani ya sasa baada ya kugawa faida kati ya UTT
na BMC.
iii) Changamoto za Mradi
Katika kutekeleza mradi huu tumekabiliana na changamoto zifuatazo:-
1.
Wakati wa uhamasishaji
mradi ulipokelewa kwa muono tofauti katika maeneo ya mradi ambapo tulilazimika
kutumia muda mrefu katika uhamasishaji.
Kwa mfano tulilazimika kuahirisha mradi
Kata ya Kitendaguro kwa kuwa jamii haikupokea mradi kwa mtazamo chanya.
2.
Baadhi ya watu
kutojitokeza wakati wa kufanya uthamini.
3.
Kuchelewa kulipa
fidia kwa baadhi ya watu kutokana na migogoro ya kifamilia.
4.
Upimaji kuvuka
eneo lililokadiriwa kulikopelekea wamiliki wa ardhi 280 maeneo yao kutwaliwa na
mradi bila kulipwa fidia katika awamu ya kwanza.
5.
Kasi ndogo ya
kulipia viwanja iliyopelekea kuongeza muda kulipia viwanja.
6.
Uwepo wa kesi za
malalamiko ya fidia kwa baadhi ya maeneo.
iv)
Ufumbuzi wa Changamoto:
(1) Kutafuta fedha kiasi cha TShs. 768,496,379.50
kuwalipa fidia wananchi 280 ambao ardhi yao iliingia kwenye mradi bila
matarajio. Mazungumzo yameanza kati ya BMC na UTT yako hatua za mwisho kuona
namna bora ya kuwalipa wathirika wa mradi huo.
(2) Kuendelea kuhamasisha
ununuzi wa viwanja.
(3) Kuendelea kutoa elimu na kutatua mgogoro pale unapojitokeza katika eneo la mradi.
v) HITIMISHO:
Ni
matumaini ya Halmashauri kuwa malengo ya mradi yatafikiwa. Kupitia mradi huu Halmashauri inatarajia
kupata gawiwo la Shilingi bilioni 2 (TShs. 2 bilioni). aidha, faida ya muda
mrefu ya mradi huu ni kuongezeka kwa mapato ya Halmashauri kupitia 20% ya Kodi
ya ardhi na kodi ya majengo (property
tax).
C: UJENZI WA KITUO CHA MABASI
Halmashauri katika kuboresha huduma ya usafiri wa
mabasi na kupambana na changamoto ya
kuwa na kituo kidogo cha mabasi (kisichokidhi mahitaji) imeamua kujenga kituo
kipya cha mabasi katika eneo la Kyakailabwa
Kata ya Nyanga.
i) Shughuli zilizofanyika:
·
Kuainisha eneo la
mradi. Eneo lina ukubwa wa mita mraba
91,200
·
Kulipa fidia kwa
wamiliki 8 ambao ardhi yao ilitwaliwa, ambapo jumla ya Shilingi za Kitanzania
milioni 22 zimelipwa.
·
Kusafisha eneo na
kujaza kifusi katika eneo la ujenzi kwa gharama ya Shilingi za Kitanzania milioni 134 (TShs.
134milioni).
·
Kushirikiana na
Mzinga Co operation kuandaa Andiko la Mradi, ambapo ujenzi wa kituo cha kisasa
utakaojumuisha eneo la kupaki mabasi, eneo la kuegesha malori, Kituo cha
mafuta, jengo la kupumzikia wasafiri, Super market, jengo la kukatia ticket,
Utawala na majengo mawili ya vitega
uchumi ni sehemu ya mradi tarajiwa.
Kwa kushirikiana na Shirika la Mzinga Halmashauri
inaendelea na mazungumzo na UTT kuomba kufadhili mradi huu. Awamu ya kwanza itahusisha ujenzi wa Uzio,
ujenzi wa eneo la kupaki mabasi na malori, jengo la kukatishia ticketi, jengo
la kupumzikia wasafiri na Vyoo. Aidha,
Shirika la Mzinga watajenga Supermarket. Makadirio ya mradi huu (phase 1) ni TShs.
bilioni 5 bila kuhusisha gharama ya Supermarket itakayojengwa na Shirika la
Mzinga.
Changamoto
i)
Kuwepo kwa kesi
mahakamani ya wananchi wawili waliyokataa kuchukua fidia.
ii)
Kupata wabia
katika utekelezaji wa mradi ambao ni
mkubwa wa wenye kukadiriwa Shilingi bilioni 26 (TShs. 26 bilioni).
iii)
Maboresho ya barabara
kwa kiwango cha lami kutoka Kyakailabwa kwenda Buhembe ambayo ni barabara
muhimu kuingia stendi mpya.
Ufumbuzi
wa Changamoto:
(i) Kuomba
kesi isikilizwe nje ya Mahakama na wadai wamekubali kufanya hivyo.
(ii)
Kuendelea kuiomba serikali kutekeleza ahadi ya Rais ya kujenga barabara
ya Kyakairabwa kwa kiwango cha Lami.
(iii)
Tunatarajia kwamba kukamilika kwa awamu ya kwanza ya ujenzi (Phase I)
kutakuwa chachu ya kushawishi wafadhili weingine kujitokeza.
HITIMISHO:
Mradi huu una matumaini ya kutekelezwa na unatarajia
kupandisha mapato ya Halmashauri ya stendi kutoka TShs. 156 milioni hadi 1.095
bilioni kwa mwaka.
D: MRADI WA KUOSHA MAGARI
Mradi huu umeibuliwa kutokana na ukodishaji wa eneo
la Karakana la Halmashauri (Emergent Project).
Mradi huu unahusisha Ubia kati ya halmashauri ya Manispaa na Kampuni ya
ACE Chemical Ltd yenye makao makuu Morogoro na tawi lake lipo mjini Bukoba. Hadi sasa mradi umegharimu TShs. Milioni 297
fedha zote zimetolewa na ACE Chemical Ltd.
Changamoto
1. Pamoja na
kuwa mradi umetekelezwa kwa 75% wenye magari
hawajahamasika kuoshea magari kwenye kituo cha Kisasa.
2. Kuendelea
kuwepo kwa vituo holela vya kuoshea magari.
3. Mtazamo
hasi wa jamii kuhusu mradi huo.
4. Kuchelewa
kusaini mkataba wa ushirikiano wa uendeshaji kutokana na kituo kutokamilika kwa
wakati. Maudhui ya mkataba yanategemea
kujulikana gharama halisi za ujenzi wa kituo hiki. Mkataba utakuwa na sura ya mradi kujilipa na
hatimae kubaki mali ya Halmashauri (BOT).
Ufumbuzi
wa Changamoto:
1.
Kuendelea
kuhamasisha waosha magari kutumia kituo kipya cha kuosha magari.
2.
Kuhamasisha vijana
kuchangamkia fursa ya ajira katika kituo hiki.
3.
BMC na ACE
kuendelea kuweka mazingira rafiki kuwezesha kituo kufanya kazi kama ilivyo
kusudiwa.
HITIMISHO:
Kupitia mradi huu mapato ya Halmashauri yanatarajia
kuongezeka kutoka TShs. Milioni sita hadi milioni 22 kwa mwaka na aidha
kuongeza ajira ya vijana.
E: MRADI WA SOKO
Mradi wa ujenzi wa Soko jipya ni utekelezaji wa moja
ya ahadi za Mbunge katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. Aidha,
ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa uboreshaji wa maeneo ya katikati
ya mji kama ilivyo kwenye mpango mkakati wa kuendeleza mji wa Bukoba wa mwaka 2008 – 2028.
i) Shughuli zilizokwisha fanyika
·
Halmashauri kwa
njia ya zabuni ilimteua Mkandarasi Mshauri OGM kuandaa Andiko la Mradi la awali
kwa gharama ya Tshs. 522 milioni.
·
Andiko la awali na mchoro huo viliwasilishwa na
kukubaliwa kwenye kikao cha Baraza la
Madiwani cha tarehe 18/10/2011 kwa ajili ya kuendelea na mchakato wa kuuza
andiko.
·
Kupitia kwa
Mtaalam Mshauri (Promoter) (PTSL) Halmashauri ilifanikiwa kufanya mazungumzo na
TIB kuhusu kufadhili ujenzi wa Soko
ambapo mnamo tarehe 16/04/2012 kwenye kikao cha Baraza la Madiwani ulisainiwa
mkataba wa malipo ya Mkandarasi Mshauri
kati ya TIB na BMC.
·
Aidha Halmashauri
iliingia mkataba wa makubaliano na TIB wa
kumtamtaka mkandarasi mshauri atekeleze majukumu yafuatayo:-
·
(i)
Kufanya utafiti
yakinifu (Feasibility study).
(ii)
Kutengeneza
Business Plan .
(iii)
Kuandaa gharama za
mradi (Bill of Quantities)
(iv)
Kuandaa andiko la
zabuni (Tenda /document)
Aidha mnamo tarehe 23/4/2012 ulisainiwa mkataba wa
Techinical Assistant Agreement siku hiyo
pia ulisainiwa mkataba wa mkopo wa
Shilingi milioni 200 toka TIB kwenda BMC kuwezesha Halmashauri kutekeleza
majukumu yake kwenye mkataba wa Technical Assistant Agreement, na kwamba fedha
hizo zingetumika kama sehemu ya malipo kwa Mkandarasi Mshauri
OGM.
Aidha mkataba huu ulikuwa na kipengele cha ruzuku ya
TShs. 90 milioni kutoka TIB kwa ajili ya malipo ya Mkandarasi Mshauri.
·
Mpango Kazi wa Upembuzi yakinifu.
-
Mpango Kazi
uliyokubaliwa na pande zote tatu (TIB, BMC na OGM) ulikuwa kwamba andiko la mradi
likamilike ifikapo Machi, 2012 tenda itangazwe April, 2012 na iwe imegawiwa
June, 2012 na ujenzi wa Soko uanze Septemba, 2012.
Aidha kazi nyingine zilizofanyika ni pamoja na:
·
Kubainisha maeneo
kuhamishia wafanya biashara ambapo maeneo yaliyobainishwa ni jengo la CCM mkoa, Soko la
Nyakanyasi, Machinjiyo ya zamani,
Kashozi Road na eneo la CCM Miembeni.
·
Kutengeneza
michororo na BOQ za uendelezaji wa maeneo hayo, ambapo Shilingi za Kitanzania
milioni 212 zitahitajika kukamilisha.
·
Kutafuta fedha za
kuwalipa wenye mikataba na Halmashauri ya uendelezaji/ukarabati Sokoni hususani
mabucha takribani Shilingi za Kitanzania
milioni 19.
·
Kuorodhesha
wafanya biashara watakaohamia maeneo mapya na kuomba nafasi kwenye Soko jipya
ambapo fomu 1,297 zimechukuliwa, kujazwa
na zimerejeshwa.
·
Kuendelea kutoa
elimu kwa wafanyabiashara ya umuhimu wa kuwa na Soko la kisasa.
ii) Changamoto
1.
Kikundi cha wafanya biashara kufungua kesi mahakamani.
- Kikundi cha wafanya abiashara kilitoa kusudio
na hatimaye kufungua kesi ya kupinga
ujenzi wa Soko kwa madai makuu mawili.
a)
Halmashauri
isiwahamishe Sokoni hadi imeandaa maeneo mbadala ya wao kufanyia biashara wakati wa ujenzi.
b)
Au kuwafidia Shilingi za Kitanzania bilioni 5 (TShs. 5.0 bilioni)
Kesi hii itasikilizwa mwezi Machi na hali hiyo
kupunguza kasi ya ujenzi wa Soko.
2. Kuchelewa kwa mkandarasi Mshauri kuchukua vipimo
vya udongo kulikopelekea kuchelewa kukamilika kwa Andiko la Mradi. Timu ya
Mkandarasi Mshauri iliwasili Bukoba tarehe 25/11/2012 kufanya kazi hiyo, hata
hivyo kikundi cha wafanya biashara waliyofunguwa kesi mahakamani kiliwazuia kufanya kazi hiyo.
3. Halmashauri kuchelewa kurejesha mkopo TIB wa
Shilingi milioni 200 (TShs. 200 milioni)
uliyotakiwa kurejeshwa tarehe 31/10/2012 ambapo hadi mwezi Novemba 2012 kiasi
cha Shilingi milioni 20 tu (TShs.20
milioni) zilikuwa zimerejeshwa.
Ufumbuzi
wa Changamoto
Halmashauri kutafuta fedha TShs.450 kwa ajili ya:
·
Kulipa deni la TIB TShs. 200 ambalo limeiva muda
wake wa kurejeshwa.
Halmashauri imewasiliana na TPB kukopa fedha hizo
ambazo zitarejeshwa kupitia faida ya mradi wa upimaji viwanja.
·
TShs. 250 milioni
kwa ajili ya kuboresha maeneo ya kuwahamishia wafanya biashara (TShs. 212 milioni),
kurejesha fedha za kimkataba kwa wenye bucha waliyoboresha bucha hizo kwenye
Soko linalotarajiwa kuboreshwa. (TShs.
19m.) na kulipia gharama za GEOTECH Shilingi
milioni 19.
·
Kuendelea na
mchakato wa manunuzi kuwapata wakandarasi wa kuboresha maeneo mbadala.
·
Kuendelea kutetea
maslahi ya Halmashauri katika kesi iliyoko Mahakama Kuu.
HITIMISHO:
Endapo mradi huu utatekelezwa kama ulivyopangwa
mapato ya Halmashauri yatokanayo na Soko yatapanda kutoka wastani wa TShs.
Milioni 168 kwa mwaka hadi bilioni mbili
kwa mwaka. Napenda kusisitiza kwamba
Halmashauri haijangia mkataba wa ujenzi wa Soko kwa sababu mchakato wa upembuzi yakinifu haujatufikisha
hatua ya kutangaza zabuni ya ujenzi.
AHSANTENI KWA KUNISIKILIZA
HAMIS J. KAPUTA
MKURUGENZI WA MANISPAA
HALMASHAURI YA MANISPAA BUKOBA
No comments:
Post a Comment