Friday, October 5, 2012

ZITTO KABWE ACHANGIA BIMA YA AFYA KWA MJANE WA MWANGOSI NA MWANAWE KUPITIA NSSF


KATIKA siku ya mwisho ya harambee ya kumchangia mjane wa marehemu Daud Mwangosi, Ndugu Zitto Kabwe amejitolea kumchangia mjane wa marehemu kwa kumlipia ada ya uanachama wa Mfuko wa Hifadhi ya Kijamii (NSSF) kwa kila mwezi na kwa miaka mitatu mfululizo.

" Nimeona nami niunge mkono harambee hii.Pamoja na michango ya fedha iliyotolewa kumsaidia mjane kuanzisha mradi wa kujikimu, mimi naona ni muhimu pia mjane akawa na hakika ya huduma ya afya yake na watoto wake wanne. Hivyo, mchango wangu utakuwa ni kwenye eneo hilo Bima ya Afya na kwa miaka mitatu." Anasema Zitto Kabwe alipoongea na Mjengwablog.com, mtandao wa Kijamii ulioratibu harambee ya mjane wa Daud Mwangosi.


Hii ni mara ya pili kwa Ndugu Zitto Kabwe kuchangia kwenye masuala ya kijamii kupitia mtandao wa kijamii wa Mjengwablog.com, mara ya kwanza ni alitoa mchango wake pale Mtandao wa Mjengwablog.com ulipoendesha harambee ya kuwachangia watoto wa Somalia waliokuwa katika hatari ya kufa kwa njaa.


Katika harambee iliyomalizika Jumapili ya Septemba 30 mwaka huu na iliyochukua kipindi cha mwezi mmoja,zaidi ya shilingi milioni tano na nusu zimekusanywa.


Mchango huo wa Ndugu Zitto Kabwe una maana mjane wa marehemu ataweza kuwa na hakika ya yeye na watoto wake wanne kupata huduma za afya bila kufikiria malipo kwa kipindi cha miaka mitatu. Baada ya hapo,michango ya mjane huyo ya kila mwezi kwa mfuko huo wa hifadhi ya kijamii ( NSSF) ambayo atakuwa akilipiwa na Ndugu Zitto Kabwe itakuwa ni malimbikizo ya akiba yake ambayo mjane atakuwa na uwezo wa kuichukua kama akipenda. Kwa sasa mjane wa Daud Mwangosi hayuko kwenye utaratibu wowote wa Bima ya Afya, kwake yeye na wanawe.


Harambee ya mjane wa Daud Mwangosi iliyoendeshwa kwa uwazi kwa njia ya MPESA, TigoPesa, Airtel Money, NMB Mobile na Western Union ilimwezesha mchangiaji kuliona jina lake na mchango wake kwenye orodha ya wachangiaji iliyokuwa ikiwekwa mtandaoni kila siku. Michango ilikuwa ni hiyari, hakuna aliyeombwa kutoa na utaratibu haukuruhusu ahadi za kuchangia, bali, mwenye nacho alitoa na hapo hapo kuorodheshwa kama mchangiaji. Utaratibu haukuruhusu pia michango iliyofungamana na siasa za vyama.


Hatua hiyo ya uwazi na kutanguliza ubinadamu na si itikadi kwenye uchangiaji imechangia kupelekea Watanzania wengi wa kada zote, kwa namna moja au nyingine kushiriki kwenye kuchangia. Kuna waliochangia shilingi elfu moja na kuna waliochangia mpaka shilingi milioni moja.


Ari hii ya Watanzania kujitolea kusaidiana kwenye hali kama iliyomkuta mjane wa Daud Mwangosi imedhihirisha umoja na upendo tulionao kama Watanzania, na pia imeonyesha jinsi tunavyoijali amani yetu na hivyo jamii, kupitia michango hii, imeonyesha pia kwa vitendo, dhamira ya kulaani kwao vitendo vya maovu na vinavyotokana na matumizi ya nguvu yasiyo ya lazima kama kile kilichomtokea mwandishi Daud Mwangosi.


Baadhi ya watu maarufu katika jamii waliojitokeza kwa hiyari yao kumchangia mjane wa Daud Mwangosi kupitia mtandao wa kijamii wa Mjengwablog.com ni pamoja na Shy- Rose Bhanji, Ananilea Nkya, John Bukuku ( Mmiliki wa Fullshangwe.blog) na Ndugu Mobhare Matinyi aliyepata kuwa mhariri wa gazeti la Majira.


Michango kwa mjane wa Daud Mwangosi itaingizwa kwenye akaunti ya mjane ya CRDB, Iringa leo alhamisi, Oktoba 4, 2012. Vielelezo vya kibenki vitawekwa kwenye mtandao wa Mjengwablog.com kwa kila mmoja kuona jumla iliyowasilishwa kwa mjane na orodha ya majina ya wachangiaji.

No comments: